Thursday, November 18, 2010

AHAMED KHALFAN GHAILANI, MTANZANIA MWENYE KESI YA MAUWAJI.

Mshukiwa wa ugaidi, Ahmed Khalfan Ghailani ametajwa jana na mwendesha mashtaka katika mahakama ya Manhattan nchini Marekani kama ‘muuaji wa halaiki’.

Ghailani anatuhumiwa kuhusika katika miripuko ya mabomu mwaka wa 1998 katika balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania.

Katika mchango wake wa mwisho katika kesi hiyo, mwendesha mashtaka wa mahakama ya Manhattan, Harry Chertoff alisema Bw Ahmed Khalfan Ghailani ambaye alikuwa ameketi viti kadhaa upande wake wa kushoto, ni muuaji wa halaiki ambaye ana alama ya damu ya mamia ya watu mikononi mwake.

Ghailani, Mtanzania anayetokea Zanzibar, ana umri wa miaka 36 na anahusishwa pakubwa na kupanga miripuko ya mabomu katika balozi za Marekani mjini Nairobi na Dar es Salaam mwaka wa 1998 iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Mshukiwa huyo alikana makosa hayo na anahusishwa pakubwa na mtandao wa Al-Qaeda katika kanda ya Afrika mashariki.

Kesi yake ni ya kwanza ya washukiwa waliokuwa wameshikiliwa katika gereza la Guantanamo nchini Cuba, kusikilizwa katika mahakama ya kiraia.

Mahakama ya Manhattan ni hatua chache kutoka katika jengo la mnara wa World trade centre ambapo shambulio la kigaidi la Septemba 11 mwaka 2001, lilitekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Wachunguzi wanalinganisha uhusiano huo kama hatua kubwa ya kutanzua kitendawili cha mashambulizi ya kigaidi.

Rais Barack Obama wa Marekani alitoa amri ya kufungwa kwa mahakama ya kijeshi ya Guantanamo na washukiwa wanaoshikiliwa wafunguliwe mashtaka katika mahakama ya kiraia.

Azimio hilo lilipingwa vikali na wachunguzi kadhaa wakidai kwamba uzito wa kesi hizo za ugaidi haufai kushughulikiwa katika mahakama za kiraia.

Jaji, Lewis Kaplan amesema kesi hiyo inaweza kuendelea hadi mwakani.

Khalfan Ghailani alikamatwa mwaka wa 2004 akiwa nchini Pakistan.

No comments:

Post a Comment