Thursday, November 18, 2010

HARAKATI za serikali kuboresha huduma za afya, zimepata msukumo mpya baada ya Shirika la Pharm Acces la Uholanzi, kutenga zaidi ya Euro 2 milioni sawa na Sh400 bilioni kuboresha hospitali na zahanati binafsi nchini.
Pia, Pharm Acces limeanzisha mpango wa bima ya afya kwa watu walio katika sekta isiyo rasmi, tayari limeanza kutoa huduma hizo Dar es Salaam na Arusha kwa kushirikiana na Chama cha Watoa Huduma za Afya nchini (APHFTA).

Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mipango wa Pharm Acces, Geert Haverkamp na Meneja Mipango wa APHFTA, Dk Samwel Ogillo, walisema chini ya mpango wa utoaji mikopo, wamiliki wa hospitali binafsi watapatiwa mikopo nafuu.

Haverkamp alisema Tanzania ina changamoto kubwa katika bajeti ya afya na upatikanaji fedha, huku akionyesha tofauti na nchi za Ulaya na Marekani, mtu mmoja hutengewa Sh1 milioni kwa afya kila mwaka, Tanzania hutengewa Sh22,000.

Kutokana na hali hiyo, alisema Pharm Acces imejipanga kuwezesha watoa huduma za afya kupitia sekta binafsi ili kuboresha nyenzo na huduma wanazotoa kwa wananchi.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Pharm Acces imetenga Euro 2 milioni kusaidia kuboresha huduma za afya kupitia sekta binafsi.

Naye Dk Ogillo alifafanua kuwa uwezeshaji huo, utakwenda sanjari na utoaji mafunzo ya biashara kwa wamiliki wa zahanati, na hospitali binafsi.
Alisema vigezo vitakavyowezesha wamiliki na watoa huduma za afya kupata mikopo ni uanachama wa APHFTA na yule anayetunza vitabu vya hesabu za zahanati, kilinini au hospitali yake.

No comments:

Post a Comment